DIBAJI
Kumekuwa na maelezo
na sababu nyingi zinazotolewa kuhusu umaskini wa jamii ya Tanzania. Wako
wanaosema kukosekana kwa uwekezaji ni chanzo kikubwa cha uchumi wetu kuyumba.
Lakini katika
kuvutia uwekezaji huo, lazima tujiulize, je fursa zinazojitokeza za kiuchumi
zina uwezo wa kubadilisha uchumi wetu kutoka katika hali duni?
Changamoto nyingine
inayosemwa ni juu ya Teknolojia. Je teknolojia hii hasa hasa ya kutoka nje inasaidia
uchumi wetu kukua? Na kama ni hivyo ukuaji wake una changamoto gani?
Changamoto za elimu,
mathalani ni elimu gani ambayo inatolewa na ina manufaa gani kwa umma?
Lakini pia,
hatudhani kuwa kuna matatizo au sababu nyingine ambazo zinachangia suala zima
la umaskini wa Tanzania na kuwa ni sababu hizi tunaishi nazo na ni sehemu ya
kawaida ya maisha ya watu?
Kupitia kitabu hiki
nitajitahidi kuainisha sababu mbadala za Tanzania na Watanzania kuwa maskini
katika nchi yenye utajiri mwingi wa mali asili kuliko nchi nyingi
zilizoendelea.
SURA YA KWANZA
MATUMIZI YA LUGHA
ISIYO YA ASILI KWA MTANZANIA -
KISWAHILI
Kiswahili ni lugha
sasa ya kimataifa. Ni lugha ambayo wengi hatuwezi tena kukataa kuwa ina mashiko
kijamii na kimataifa na mikakati ni kuifanya iwe lugha kuu hapa Afrika. Wazo
kama hili ni jema sana. Litaifanya Afrika iwe na lugha yake pekee ambayo
imetokana na eneo la Afrika na ambayo imeweza kutumiwa na jamii pana.
Nchi ya Tanzania ina
uzoefu mkubwa wa matumizi ya Kiswahili hasa kutokana na kuwa na pwani kubwa ya
Afrika Mashariki, na inavyosemekana ndiyo imekuwa kiungo cha kuleta umoja na
amani iliyopo leo. Wakati wa kupambana na wakoloni inasemwa Kiswahili kilikuwa nguzo
moja wapo ya kuwaunganisha Watanganyika wakati huo. Na katika Mapinduzi ya
Zanzibar, Kiswahili pia kilitumika kuwaunganisha Wazanzibar.
Kiswahili kina mengi
sana ya sifa kama ilivyo kwa uwepo wa lugha nyingine duniani. Kusudi langu la
kuandika kitabu hiki sio kueleza yale ambayo tayari yamekuwa yakielezwa kuhusu
Kiswahili na umuhimu wake katika maisha yetu ya kila siku.
Bali, ni kuona namna
lugha inavyoweza kuwa na athari pana katika maisha ya kila siku ya jamii
inayoitumia. Kiswahili kinabeba dhana ya uswahili. Uswahili unabebwa na dhima
ya Mswahili. Mswahili ni nani?
Tukijaribu kurudi
nyuma katika maisha ya makabila mbalimbali na hasa yale kwa namna moja au
nyingine yalitoa mchango katika kukitengeneza Kiswahili (makabila ya pwani)
ambayo yalipata bahati kukutana katika shughuli mbalimbali za kijamii, na
Waarabu tunapata kizazi kipya hiki cha Mswahili.
Kiswahili kimsingi
kimechangiwa kwa karibu sana na Waarabu, Wahindi na makabila mengi ya Pwani ya Afrika
Mashariki. Makabila yetu ya pwani, Waarabu na Wahindi hawa kimsingi walijua
lugha zao za asili, yaani lugha za makabila yao, kwa Waarabu - Kiarabu na kwa
Wahindi - Kihindi. Wote hawa walishirikiana katika biashara, kuoleana na
kadhalika. Katika kutafuta kuwasiliana, ndipo Kiswahili kikazaliwa. Kimeendelea kupanuka kutokana na mwingiliano
wa jamii nyingine za makabila na nchi nyingine ijapokuwa hakijapoteza ile dhima
yake ya uswahili.
Jamii iliyozaliwa hapa ilitengeneza
ustaarabu wa namna yao ya kuishi na kufanya shughuli zao za maendeleo. Kama
ilivyokuwa Uarabuni kuna mafuta, na Pwani kuna mazao ya samaki yaani kuvua, pia
pwani kuna mazao ya muda mrefu kama minazi, mikorosho na miembe, mwingiliano
huu ukaleta ile dhana pwani shughuli nyingi zinasimamiwa na “uasilia” wa
MAZINGIRA (Waarabu - Mafuta).
Je ni aina gani ya biashara au shughuli gani
walizokuwa wanafanya? Na baada shughuli za uzalishaji mali ambazo kimsingi ni uchimbaji
mafuta kwa Waarabu (na hapa hufanyika na makampuni sio mtu binafsi na kutokana
na mazingira hakuna uzalishaji wa moja kwa moja wa shughuli nyingine –
UKAME wa jangwa) na kuvua kwa makabila
ya pwani, basi walijipumzisha huku wakicheza michezo mbalimbali. Je mfumo wa
michezo yao ulikuwa au ukoje mpaka leo?
Utamaduni uliozaliwa hapa ni ule wa
kuitegemea asili (nature) ikupatie kile unachokitafuta. Kwa kuwa uwepo wa
mafuta ni wa muda mrefu, vivyo hivyo kwa samaki katika bahari na maziwa,
Mswahili aliyetengenezwa hapa alijikuta akiwa mtu mwenye kusubiri, kujenga
matumaini ya kujua maisha yanaendelea hakuna tatizo. Utamaduni ambao jamii
haina uwajibikaji wa moja kwa moja.
Alilima mazao yanayotoa mazao kwa muda mrefu
kama minazi, korosho, maembe na kadhalika.
Hakuwa tayari kufanya shughuli ambayo kwake
ni shulba na ambazo hata baada ya kuja kwa wazungu walipoambiwa wazifanye
waliona adhabu kama kilimo cha katani na mazao mengine, utengenezaji wa miundo
mbinu n.k.
Ndipo katika Kiswahili tunakutana na neno pole
kwa kazi! Kwa sababu kazi haikuchukuliwa kama kitu chema, ni cha kuudhi na
kinachofanywa na yule mwenye matatizo makubwa katika maisha yake. Asiye na
matatizo hatakiwi kufanya kazi na akionekana ni alama tosha kuwa ana shida
katika maisha yake.
Mfumo wa kufikiri kwa mtu aliyetokana na
uswahili (Kiswahili kikiwa ndiyo msafirishaji wa maadili na teknolojia), hakuashirii
msukumo wa uzalishaji katika kiwango cha juu bali kuwa mtu mwenye subira –
“Subira yavuta heri”. Je ni kweli katika maendeleo tuwe na subira? Na je heri
inatafutwaje?
Tunapozunguza leo, tukienzi Kiswahili ni
lazima tukichunguze kwa makini pamoja na kuleta umoja na amani, je vitu hivi
vimetupa manufaa gani? Ni yale yakutoona damu ikimwagika kutokana na matumizi
ya silaha?
Je mbona damu nyingi zaidi inapotea kutokana
na uvivu na uzembe unaofanywa na hao ambao wamekuzwa na Uswahili na Kiswahili
na sababu kuu ni mfumo wa Kiswahili katika Maisha?
Je, ni
wangapi wanashindwa kutimiza ndoto zao kwa kukumbana na Uswahili katika
utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku. Je, Uswahili unanasibishwa na nini;
sio uvivu, uzembe, majungu, wivu unatokana na wengi kutopenda kazi hivyo
kunyang’anyana kidogo kilichopo?
Je, ni kweli kuwa
watanzania wengi hawana uwezo wa kushindana katika Afrika Mashariki kutokana na
lugha ya Kiswahili au na tabia za Kiswahili na Uswahili? Je nchi nyingine jamii
zinazozungumza Kiswahili wanachukuliwaje mathalani Burundi, Rwanda, Uganda na
Kenya? Unapita sehemu fulani ya nchi unasikia “hapa ni kwa Waswahili”!!
Wanakuwa na vigezo gani?
Ndipo sasa tunafikia
suluhisho la kutafuta mfumo mwingine wa mawasiliano, usiotokana na Kiswahili,
wenye asili ya kiafrika, unaweza kutoa picha ya msukumo wa asili yetu kufanya
kazi kwa juhudi na kuwa na msukumo wa “performance”. Kuwa tunatamani kupata
maendeleo, huku mfumo wetu hauna uasilia wa kimfumo kutusukuma kufanya kazi kwa
weledi, kwa juhudi na maarifa.
Aidha, naomba
tujadiliane kwa hoja ili tuone kama haya ninayoleta kwenu yana mashiko au laa!
Na tufikie wote kuamua mustakabali wa taifa.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.