Tuesday, August 25, 2015

MUENDELEZO WA KITABU CHA SABABU MBADALA ZA UMASKINI WA TANZANIA - SURA YA PILI

SURA YA PILI KUUA NGUVU ZA ASILI ZA MAKABILA YETU. Kama nilivyosema katika dibaji ya kitabu hiki, maandishi yangu hayazingatii sana utafiti wala utaalamu wa uandishi na wala rejea zozote, ni mawazo binafsi ambayo wengine wanaweza kukubali au kukataa ni katika mitazamo tuu. Tukijaribu kurudi nyuma katika maisha ya jamii nyingi za waafrika hasa hapa Tanzania, tunakutana na tamaduni mbalimbali za makabila mbalimbali zilizolenga katika kuheshimiana, kushirikiana, kupendana na kulindana. Makabila haya yalikuwa na taratibu mbalimbali zinazosimamia maendeleo yao ya kijamii, mifumo ya uongozi, na namna mbalimbali ya kukabiliana na majanga kama ya njaa, moto, magonjwa n.k. Kila kabila kwa asili yake lilikuwa na namna lilivyomuandaa mtoto hadi ujana ili akubalike kuwa mwanajamii wa kawaida. Alipimwa kwa mambo mengi ya ushujaa, uchapa kazi, ubunifu, unadhifu, uadilifu na weledi katika utendaji wa shughuli za maendeleo. Jamii ikimpata kijana kama huyu itamkabidhi mke ambaye naye atachaguliwa kulingana na vigezo hivyo. Changamoto kwa hiyo ni uwezo wa kila mwanajamii kuwa mzalishaji kwa kuwa jamii iliwategemea vijana hawa moja kwa moja. Makabila kama ya Masai, Wachaga, Wasukuma, Wahaya, Wakwere, Wamakonde, Wazigua na mengine yalikuwa na namna yalivyokuwa yanaratibu ukuaji wa vijana wake hadi kuwa watu wa wazima ambao sasa wangeweza kushiriki katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya kijamii katika kujitafutia maendeleo. Leo kwa kuwa jamii pana ya Tanzania inadai imeendelea, na hapa ikumbukwe kuwa hakuna jamii ya Watanzania. Jamii hii inazaliwa kutoka katika makabila yaliyoko Tanzania chini ya mwavuli wa tamaduni na mila, desturi na maadili ya makabila husika, tumekuwa na dhana inayoitwa kupambana na ukabila. Dhana hii inatiliwa nguvu na ukweli kuwa mwanadamu anapenda kuhusiana sana na yule anayemfahamu, aliyekaribu nae na ambaye anaamini kati yao ni wamoja. Ndio maana ukiwa CCM unamuona Mwana CCM ni ndugu yako, ukiwa CHADEMA au CUF nakadhalika. Ukiwa Mwislam vivyo hivyo, na kwa makundi mbalimbali ya kijamii. Kinachoshangaza hapa ni mikakati ambayo inawekwa mahususi katika kuangamiza kinachoitwa Ukabila. Lengo likiwa ni kutengeneza jamii moja pana inayoitwa ya Watanzania. Katika makabila haya tumeona miundo mingi ya usimamizi wa maadili inavyosimamiwa na mila na desturi kwa watu wa makabila hayo. Je mila na desturi zitakazoisimamia Tanzania ni zipi? Ndio maana Ulaya na mabara mengine kumekuwa na mmomonyoko wa maadali kwani mdumo wa kijamii umeparaganyika. Hajulikani baba, mama, babu, bibi, mtoto au mjukuu. Hii inatokana na wao kuua mfumo wa asili wa mahusiano ya kijamii na kuunda hiki tunachotaka ambacho ni jamii iliyoondokana na ukabila. Kwa nini katika makundi mengine tunatengeneza lugha ya kuvumiliana na sio kwenye makabila. Kwenye dini utasikia tujenge uvumilivu, kwenye vyama vya siasa tujenge uvumilivu, kwenye kabila – tutokomeze ukabila. Je manufaa yake siku za mbeleni ni yapi? Tujaribu hata kuangalia katika wakati tulionao. Vijana wengi wamechanganyikiwa, hawajui tena asili ya utamaduni wanaotakiwa kufuata. Leo kwa kuwa dhana ya ukabila imewaingia kama sumu hawataki kufahamu hata mila na desturi zao ambazo ndizo zingewajengea taswira ya Uafrika wao. Hawana urithi wa kijamii unaotokana na mwendelezo wa fikra zenye ushawishi wa kimwamko. Mathalani wachaga ni wafanyabiashara lakini kwa leo vijana wao hawataweza tena kufanya biashara kama ilivyokuwa kwa wazazi wao. Wamasai kwa mfano ni wafugaji, lakini leo hawawezi tena kuendana na mfumo uliowapa nidhamu na kujambua na kuthamini kile kinachomilikiwa na jamii, ambacho ni mifugo. Katika ufumaji mpya wa makundi haya ya kijamii, ili yaendane na mwenendo huu wa kisasa wa kuua ukabila, lazima tuwe makini kwani ndani yake tunaua teknolojia za asili, ubunifu, nidhamu, maadili, mila na desturi kama tutakavyoona katika sura ijayo, na mwisho ni kuwa na Taifa linalojiita moja lakini likiwa limeparaganyika kama nchi za Ulaya zilivyo leo. Kuparaganyika huku tuna maana gani? Ni pale ambapo kama jamii, hatuna tena mfumo wa malezi ya kijamii kulingana na mila na desturi, bali tumebaki tunatengeneza taasisi za mpito za malezi kama vile Jeshi la Kujenga Taifa na nyingine. Je tuulizane, JKT imeweza kweli kuwajengea maadili wale walio waliojiunga nalo? Mfano viongozi, wana maadili ya uongozi? Wanafahamu dhima ya utu na watu hivyo kutumikia jamii kikamilifu? au kwa mfumo wa kijamii kati ya Baba, Mama, Mtoto, Babu, Bibi, Mjomba, Shangazi, Binamu na jamii yote, taasisi hizi zina uwezo kuwajengea taswira watoto, na vijana kutambua wajibu wao?? Tutafakari kwa kina kabla ya kuingia Sura nyingine ya Kitabu hiki.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.