ELIMU NA UTAALAMU

Elimu kwa maana ya kawaida ni maarifa anayoyapata mtu, yanayomwezesha kutambua changamoto mbalimbali zinatokana na mazingira anayoishi. Katika kupambana na changamoto hizi ndipo maendeleo yake yanapopatikana. Na pia ndipo anapozalisha mbinu mbalimbali na ugunduzi unaotokana na yeye kuzitambua changamoto hizo na kuzifanyia kazi.



Dhana ya Elimu inakwenda mbali zaidi kwa kuweka aina mbalimbali za elimu na hii inazingatia sana namna elimu hizo zinavyopatikana. Aina ya kwanza ni elimu inayopatikana katika mazingira mtu anayoishi. Elimu hii hutolewa na wazazi, na kwa ujumla jamii inayomzunguka mtu. Huweza kutolewa kwa njia ya unyago, jando, hadithi, na mikutano mbalimbali ya makundi katika jamii husika.



Mtoto au kijana huandaliwa na familia, kwa kushirikiana na jamii. Maandalizi haya yanakwenda sambamba na elimu ya mazingira ambayo hutolewa na wazazi pia na wazee walioteuliwa kutokana na utaalamu wao wa masuala mbalimbali ya kijamii. Elimu hii inamwezesha mtoto huyu na baadaye kijana kutambua wajibu wake na mahitaji ya mazingira katika kuishi.



Aina nyingine ya elimu ni ile mtu anayoipata bila kujitambua. Elimu hii inapatikana kwa kuiga, ambapo mtu anajikuta anabeba baadhi ya tabia na muonekana wa watu wengine wanaomzunguka.



Aina ya tatu ya elimu ni ile ambayo wengi wanapozungumza kuhusu elimu wanailenga moja kwa moja nayo ni elimu inayopatikana darasani. Elimu hii ni ya kufundishwa na kujifunza katika mfumo wa darasa. Mwanafunzi anahudhuria masomo kwa vipindi vilivyopangwa na kwa kufundishwa na walimu ambao hutumia vifaa mbalimbali vya kufundisha na kujifunzia kama vile vitabu n.k.



Elimu hii tunasema ndiyo iliyopewa kipaumbele katika maandalizi ya miundo mbinu mbalimbali kama madarasa, kusomesha walimu wengi, kuandaa mitaala kufundisha na kujifunza, mabadiliko ya sera ya elimu, na mambo mengine mengi.



Lakini swali moja ambalo wote tunajiuliza ni je elimu bora ni ipi? Ni hii ambayo hutolewa darasani! na kama ni hiyo vigezo ni vipi ni hivi vya kuwa na walimu wazuri, madarasa ya kutosha, vitabu vya kiada na ziada vya kutosha, vifaa vya maabara vya kutosha na kwa ujumla mazingira mazuri ya kujifunza na kufindisha?



Kama vyote hivi vikipatikana, mbona wasomi wanaohitimu elimu hiyo bado wanahangaika sana kutafuta ajira? Mimi nilidhani kwa kuwa ni elimu bora basi wasomi hawa watakuwa na uwezo mkubwa wa kubuni njia mbadala tofauti na kusubiri ajira zilizoandaliwa.



Wasomi hawa wamewaachia ubunifu wale ambao hawakupata nafasi ya elimu hiyo inayoitwa bora. Hawa ndio wanaotengeneza vitu mbalimbali vinavyotumiwa na wasomi hao katika maisha yao ya kila siku kama vile bidhaa zinazotokana na ufumaji na ufinyanzi kama mikeka, vikapu, vyungu na vingine vingi. Ukiwauliza wasomi hao kama wanaweza kutengeza bidhaa hizo watakuambia hawawezi.



Maana yake ni kwamba elimu hii inamnyima mtu kuwa mbunifu katika mazingira yake kwani yeye anaandaliwa kutumia teknologia iliyoandaliwa. Yeye kama yeye hawezi kutumia maarifa aliyopata kujiajiri na ndio maana kuna jeshi kubwa sana la wasomi naosubiri kupata kazi.



Taifa kama la Tanzania linatakiwa kuweka kipaumbe sana katika elimu inayotokana na mazingira ya wananchi wake. Hii itawafanya wajue wajibu wao katika kujikomboa. Ni busara kutohoa mfumo wa elimu kutoka elimu ya asili ya watu na hii ni ile ambayo watu wanaweza kufanya shughuli mbalimbali zinazotokana na mazingira yao kama ilivyo kwa wafugaji na wakulima. Nchi ina watu wengi wanaotumia mbinu finyu za ujasiria mali lakini hawana msaada wa kutaaluma, wala uwezeshaji wa namna yeyote.



Taifa kama China kwa mfano limekuza bidha na teknologia za asili na ndio maana ina bidhaa zinazofanana na kulingana kabisa na nchi zilizoendelea ingawa nchi hiyo bado inahesabika kuwa nchi za dunia ya pili.



Kwa hiyo, swali langu mara nyingi linakuwa je tuna maana gani tuposema elimu bora? Nadhani hili linahitaji ufafanuzi wa wanazuoni, na wasomi wenyewe na kwa ujumla jamii nzima ya Tanzania