AJIRA NA KUJIAJIRI

Changamoto za ajira duniani hususani nchi za Afrika na Tanzania kwa ujumla ni kubwa. Tunaweza kujiuliza nini tatizo au chanzo cha changamoto nyingi katika ajira duniani, ikiwa ni pamoja na walioajiriwa kulalamikia ajira zao; na ambao hawana ajira kulalama kwa kukosa ajira.

Ukweli ni upi! kuwa na ajira kunakupa fikra ya ajira isiyofaa hivyo kuhitaji kutafuta ajira nyingine, na nini kinamfanya binadamu aamini ajira aliyo nayo ni mbaya? Na je wale wasio na ajira wakipewa ajira hiyo mbaya nao wataikubali? Ni maswali ambayo majibu yake yanatokana sana na hulka, tabia na tamaduni za watu.

Mathalani nchini Tanzania, tunapozungumzia ajira tuna maana gani? Je tamaduni za jamii yetu pana zinatafsiri vipi dhana ya ajira? Wengi wetu tunaamini ajira ni mfumo unaotuwezesha kupata kipato kwa njia ya malipo ya mtu kwa mtu, mtu kwa taasisi/kampuni au mtu kwa Serikali. Na hapa tunaichukulia ajira kama njia ya kupambana na matatizo ya kimaisha. Matatizo yakiisha, basi hata fikra za utendaji nazo zinapungua.

Nchini Tanzania, hadi tarehe 19 Agosti, 2015 kuna waajiriwa 2,14,1351 walio katika sekta rasmi, yaani Serikali na Sekta binafsi. Idadi ya watu kulingana na makisio ya jumla ni milioni 47.42. Je, kwa idadi hiyo ya waajiriwa, tunaweza kuieleza vipi hali ya ajira nchini?

Tunaingia katika Uchaguzi Mkuu 2015, kila chama kitanadi Sera, na mikakati mbalimbali ya kuinua hali za maisha ya watu. Moja ya changamoto kubwa ni kuwa na idadi kubwa ya watu wasio na ajira hasa vijana. Lakini sio tu tatizo la kutokuwa na ajira, bali kuifanya jamii itambue nini maana ya ajira kwa kupitia kujiajiri. Hili ni pamoja na kurasimisha shughuli nyingi za jamii, kuzipa taswira ya mfumo rasmi ili zitambuliwe, na kupata sifa aidha za mikopo, kulipa kodi n.k.

Jamii zetu kama nilivyoainishwa awali zimejikuta hazitambui wajibu wetu wa moja kwa moja kuhusu kutumia mazingira yetu vizuri katika kuzalisha fursa za ajira. Hivyo, Serikali ijayo itapaswa kuifahamu vyema jamii ya Tanzania na kubuni namna ya kuwafanya wafanye kazi kwa bidii, kuongeza tija kwa wale walioajiriwa, na kuhakikisha tunafanya mgao bora wa mapato ya serikali kwa sekta zote, na kuzuia ufujaji wowote. Taifa litabadilika.

Tukijaribu kuilinganisha Tanzania na mataifa mengine yenye mali asili nyingi kama sisi, tunajikuta tuko nyuma sana kimaendeleo. Lakini kubwa zaidi, ni mfumo wetu wa elimu ambao hautoi nafasi ya kujenga uwezo wa maarifa, ujuzi na stadi za kazi, na kuzitumia katika kuzalisha fursa za ajira.

Kama taifa, tuanze sasa kujitambua na kutambua wajibu wetu wa kufanya kazi kwa kutumia maarifa na kuwa na bidii ili tulete maendeleo ya haraka.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.