Shule ya Sekondari Jitegemee (JKT) inategemea kuwa na mahafali yake ya 24 ya Kidato cha Nne itakayofanyika siku ya Ijumaa tarehe 25 Septemba 2009 kuanzia saa 3.30 asubuhi. Mahafali hayo yatajumuisha wahitimu 523 ambao kwa sasa wameandaliwa vyema kuukabili Mtihani wa Taifa unategemewa kuanza mwanzoni mwa mwezi Oktoba 2009.
Akizungumzia Mahafali hayo, Mkuu wa Shule hiyo Maj Martin Mkisi amesema pamoja na wazazi kualikwa, waalikwa wengine ni pamoja na wakuu wa asasi za umma na binafsi zinazoizunguka shule, Makao Makuu ya JKT, wajumbe wa bodi ya shule, wageni mbalimbali kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na marafiki wa wahitimu.
Wakiongea na mwandishi huyu, wahitimu hao wameonyesha furaha yao ya namna ambavyo shule imewalea na kuwafanya wazitambue changamoto mbalimbali zinazowakabili. Walizitaja kuwa ni pamoja na mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi hasa gonjwa hatari la UKIMWI. Wamewaomba wazazi wao na jamii kwa ujumla kuhakikisha kuwa wanashirikiana nao katika mapambano haya.
Mahafali hayo yatasheheni matukio mbalimbali ya burudani, michezo, ngonjera na muziki
Mgeni wa Rasmi katika Mahafali hiyo atakuwa Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha, Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.