Tuesday, September 29, 2009
MHE SHAMSI VUAI NAHODHA: "ELIMU NI KIPAUMBELE KWA MAENDELEO YETU"
Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha amewataka Watanzania wawekeze sana katika elimu kwani ndio njia pekee ya kulikomboa Taifa kiuchumi. Aliyasema hayo katika hotuba yake aliyotoa katika Mahafali ya 25 ya Kidato cha Nne, Shule ya Sekondari Jitegemee (JKT) yaliyofanyika tarehe 25 Septemba 2009.
Alisema, "ili taifa liweze kujikwamua kutoka kwenye lindi la umaskini na maradhi, lazima lisomeshe watu wake". Alitolea mfano nchi za Rwanda, China, Malasia kuwa ni nchi zilizoweka kipaumbele kwenye elimu na sasa wanaonja matunda, kwani uchumi wa nchi hizo unakuwa kwa kasi kubwa.
Aliyataja mambo makuu mawili yanayoweza kuwa na mchango mkubwa katika kufanikiwa kwa mtu kielimu. Mambo hayo ni; maumbile ya mtu (nature) na mazingira. Alisema mtu anaweza kurithi uwezo wa kiakili kutoka kwa wazazi wake. Na hii itamjengea uwezo mzuri katika kujifunza. Katika mazingira aliyataja mambo muhimu kama miundo mbinu ya elimu (shule nzuri yenye vifaa vya kufundisha na kujifunza), walimu bora na kuwa na wazazi wenye elimu. Alitoa mfano wa Shule ya Sekondari Jitegemee (JKT) kuwa ni miongoni mwa shule bora zinazoweza kumjenga mtoto kitaaluma na kimaadili kutokana na kuwa na miundombinu bora ya kufundishia na kujifunza.
Alitoa changamoto kwa wasichana kuhakikisha wanajielimisha kwa bidii ili kuwa wazazi bora na hivyo kujenga jamii endelevu.
Mahafali hayo ya 25 yalihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe Dr. Emmanuel Mchimbi, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo Ndugu RM Mpazi, wakuu wa asasi mbalimbali na wazazi wa wahitimu.
Akitoa taarifa ya mafanikio ya Shule, Mkuu wa Shule hiyo Maj Martin Mkisi alisema kuwa shule imekuwa na mikakati ya kuinua kiwango cha elimu kwa wanafunzi wake kama vile kujisomea kwa vikundi baada ya masomo ya kawaida darasani, wanafunzi kuandika insha nyingi ili kujipa mazoezi katika kupangilia kazi na kutoa motisha mbalimbali
kwa walimu na wanafunzi ili kuongeza ari ya kufaka kazi kwa bidii.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.